
HALI ya baadaye ya zaidi ya wanafunzi milioni sita katika shule za msingi na sekondari za umma nchini imo hatarini iwapo Bunge halitatenga Sh56.3 bilioni kufadhili mpango wa Elimu ya Msingi Bila Malipo katika mwaka wa kifedha 2026/27.
Mipango ya Elimu ya Msingi Bila Malipo (FPE) na Elimu ya Sekondari Bila Malipo (FDSE) imekumbwa na changamoto za kifedha kwa miaka kadhaa, hali ambayo imeacha shule na madeni na nyingine zikilazimika kuwatoza wazazi michango ili kuziba pengo la ufadhili.
Katibu wa Elimu ya Msingi, Profesa Julius Bitok, aliwaambia wabunge kuwa, sekta hiyo ina upungufu wa Sh71.77 bilioni ambazo hazijatengwa na Wizara ya Fedha kwa mwaka wa kifedha unaoanza Julai 1, 2026.
Akijitetea mbele ya Kamati ya Elimu ya Bunge la Taifa, Prof Bitok alisema wizara inahitaji Sh8.7 bilioni ili kufadhili mpango wa FPE kwa wanafunzi 6,390,414 wa shule za msingi.
Alisema jumla ya Sh15.7 bilioni zinahitajika lakini ni Sh7 bilioni pekee zilizotengwa, na hivyo kuacha pengo la Sh8.7 bilioni. Kila mwanafunzi wa shule ya msingi hupata mgao wa Sh2,330 kwa mwaka.
“Maana yake ni kuwa, wanafunzi 3,317,948 hawatapokea mgao au wote watafadhiliwa kwa Sh1,096 pekee,” Prof Bitok alieleza.
Kwa upande wa elimu ya sekondari ya kutwa chini ya FDSE, Prof Bitok alisema kuna upungufu wa Sh23.8 bilioni baada ya wizara kupewa Sh54.6 bilioni dhidi ya mahitaji ya Sh78.4 bilioni.
Alibainisha kuwa fedha hizo zinahitajika kufadhili mgao wa Sh22,244 kwa wanafunzi 3,479,187 wa sekondari, pamoja na Sh50,772 kwa wanafunzi 20,166 wa elimu maalumu.
“Pengo hili linafanya wanafunzi 1,057,158 kuwa hatarini kukosa mgao au wote kufadhiliwa kwa Sh15,779 pekee,” alisema.
Aidha, Sekondari Msingi (JSS) ina upungufu wa Sh23.8 bilioni kwa wanafunzi 3,621,798.
Wizara ilipokea Sh30.92 bilioni dhidi ya mahitaji ya Sh54.69 bilioni, huku mgao wa kila mwanafunzi ukiwa Sh15,042.
Prof Bitok aliomba Kamati hiyo ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet, Julius Melly, kuongeza Sh71.77 bilioni kuziba pengo hilo la bajeti.
from Taifa Leo https://ift.tt/RTU6Zu8
via IFTTT