
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema hatapoteza chochote iwapo Mahakama Kuu itatoa uamuzi dhidi yake katika kesi za kupinga kuondolewa kwake afisini mwaka wa 2024, akisisitiza kuwa safari yake kuelekea Ikulu bado itaendelea.
Majaji Eric Ogola, Frida Mugambi na Anthony Mrima wanatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu iwapo kuondolewa kwa Bw Gachagua kulifanyika kwa mujibu wa Katiba.
Iwapo mahakama itaamua kuwa aliondolewa afisini kinyume cha taratibu na sheria, hatua hiyo inaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka ujao, na kumpa ushawishi mkubwa zaidi kama mwanamikakati au hata mshindani mkuu wa kisiasa.
Bw Gachagua aliondolewa afisini Oktoba 2024 baada ya kuhudumu kama Naibu Rais kwa miaka miwili chini ya Rais William Ruto.
Hatua hiyo ilisukumwa hasa na wabunge na maseneta kutoka eneo la Mlima Kenya.
Alipatikana na hatia katika mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Vyama vya United Democratic Alliance (UDA), Orange Democratic Movement (ODM) na Jubilee vilishirikiana kumuondoa mamlakani.
Kuondolewa kwake kulibadilisha kabisa mazingira ya kisiasa nchini, huku eneo la Mlima Kenya, ambalo lilimpigia Rais Ruto katika uchaguzi wa 2022, likigeuka na kuchukua nafasi ya upinzani licha ya Rais kumteua Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.
Iwapo majaji watakubaliana kuwa aliondolewa kwa mujibu wa Katiba, pande husika katika kesi hiyo zimesema zitaelekea Mahakama ya Rufaa, na baadaye Mahakama ya Juu ikiwa itahitajika.
Akizungumza Alhamisi kupitia runinga ya Inooro TV, Bw Gachagua aliwataka wafuasi wake kudumisha amani na kuwa na matumaini kabla ya uamuzi huo.
“Sheria iko wazi kabisa kwamba mradi nina kesi inayopinga kuondolewa kwangu afisini, bado nina haki ya kuwania nafasi yoyote ya umma. Uamuzi tunaousubiri Jumatatu unatoka Mahakama Kuu,” alisema.
Aliwahimiza wafuasi wake kumuombea huku wakiwa na matumaini ya matokeo mazuri, akiongeza kuwa hata kama uamuzi hautakuwa wa kuridhisha, bado kuna nafasi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu.
Bw Gachagua, ambaye tangu wakati huo ameanzisha chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), alisema hata kama hatapata nafasi ya kurejea afisini, si lazima aongoze akiwa katika wadhifa wa kuchaguliwa.
“Naweza kuendelea kuongoza kutoka nyumbani kwangu Wamunyoro, jinsi nimekuwa nikifanya tangu nilipoondolewa mamlakani,” alisema.
Aliongeza kuwa ingawa angependa kuona suala la kuondolewa kwake likifungwa kabisa, halipaswi kuondoa lengo kuu la “kuikomboa nchi”.
Kiongozi huyo alisema anahitaji kuwashawishi wakazi wa Mlima Kenya kuwapigia kura wagombea wa DCP katika uchaguzi mkuu wa 2027 ili chama hicho kipate uwakilishi wa kutosha katika serikali za kitaifa na kaunti.
Kwa mujibu wake, eneo la Mlima Kenya lilijipata mashakani kwa kosa la mwaka 2022 la kuingia uchaguzi bila chama chao chenye nguvu na bila makubaliano rasmi ya kabla ya uchaguzi na Dkt Ruto.
“Hiyo ndiyo sababu ilikuwa rahisi kuniondoa na kuwafanya viongozi wengi tuliowachagua kujiunga na wale wanaopinga maslahi yetu kama jamii na kama eneo,” alisema.
Bw Gachagua alisisitiza kuwa bado amejitolea kwa ajenda ya upinzani na kuunga mkono uteuzi wa mgombea mmoja wa kumenyana na Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.
“Ikiwa haitakuwa mimi, na iwe ni dada yangu Martha Karua au ndugu zangu Edwin Sifuna, Fred Matiang’i, Kalonzo Musyoka, George Natembeya au Eugene Wamalwa, nitakubali na kumuunga mkono,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo hatakuwa mgombea wa upinzani, atatumia familia yake na rasilimali zake zote kufanya kampeni kwa mgombea atakayeteuliwa.
Pia alisema yeye na viongozi wengine wa upinzani wako tayari kukubali matokeo ya uchaguzi wa 2027 mradi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ihakikishe mchakato wa uchaguzi ni huru, wa haki na unaoaminika.
“Hatutaki hali ambayo itawasukuma wafuasi wetu kuhisi kutoridhika kutokana na mchakato usioaminika,” alisema.
from Taifa Leo https://ift.tt/HolniIS
via IFTTT