
MAHAKAMA Kuu imezuia mwandishi Patu Santoo ole Naikumi, kuendelea na maandalizi au kuchapisha wasifu wa aliyekuwa waziri William Ronkorua ole Ntimama hadi kesi kuhusu umiliki wa mradi huo itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya watoto wa marehemu Ntimama, Lydia Ntimama na Amos Ntimama, kuwasilisha kesi wakidai mwandishi huyo alikuwa akijaribu kuchapisha kitabu hicho bila idhini ya familia.
Wawili hao, ambao ni wasimamizi wa mali ya marehemu, waliambia mahakama kuwa wao ndio wenye haki za uchapishaji wa wasifu wa baba yao na kazi nyingine zinazohusiana naye.
Mahakama ilisema walionyesha kuwa wangepata hasara kubwa isiyoweza kufidiwa kwa fedha iwapo Bw Naikumi angeruhusiwa kuendelea na mradi huo.
Familia ilidai kuwa Ntimama aliagiza Chuo Kikuu cha Maasai Mara kuanza kuandika tawasifu yake miaka kadhaa kabla ya kifo chake mwaka 2016.
Baada ya kifo chake, waliamua kukamilisha mradi huo na wakamshirikisha Bw Naikumi kusaidia.
Hata hivyo, walidai mwandishi huyo alishindwa kuwasilisha kazi aliyopewa na baadaye akadai Sh1 milioni pamoja na asilimia 20 ya mapato ya mauzo ya kitabu.
Pia walimtuhumu kwa kutangaza kitabu hicho katika mtandao wa WhatsApp bila idhini yao.
Kwa upande wake, Bw Naikumi alikanusha madai hayo akisema alifanya utafiti wake binafsi na kuwa mradi huo ulikwama kutokana na ukosefu wa fedha na usaidizi kutoka kwa familia.
from Taifa Leo https://ift.tt/IZkyehS
via IFTTT