Wataalamu watabiri Ebola itaenea zaidi

MLIPUKO wa Ebola eneo la Afrika ya Kati huenda ukaenea kuwa sawia na kiwango cha mlipuko mbaya zaidi kuwahi kuzuka kihistoria, mlipuko uliotokea Magharibi mwa bara hili mnamo 2014-2016 uliowaua zaidi ya watu 11,000, kulingana na maafisa wa afya nchini Amerika.
Kituo Kikuu cha Kudhibiti Maradhi (CDC) Amerika, Ijumaa kilichapisha uwezekano wa kutokea kwa kati ya visa 10,000 na 20,000.
Kwenye mlipuko uliozuka Afrika Magharibi, zaidi ya visa 28,000 viliripotiwa. Udadisi kutoka CDC ulisema visa huenda vikaongezeka hadi 20,000 au zaidi, kulingana na kasi ya kuwatenga watu walioambukizwa ili kudhibiti kusambaa.
Msimamizi wa mikakati ya kudhibiti visa vya Ebola, CDC, Dkt Satish Pillai, alisema pasipo mikakati thabiti ya kulinda afya ya umma, “udadisi wa kielektroniki unaashiria mlipuko wa kiwango hicho unawezekana.”
Mkurugenzi wa Kituo cha Mlipuko katika Chuo Kikuu cha Brown, Amerika, Jennifer Nuzzo, alisema mfano huo “unathibitisha kile tumehofia tangu mwanzo: mlipuko huu unafuata mkondo hatari” ikiwa juhudi zaidi hazitatumika kukomesha kusambaa kwake.
Lakini alitahadharisha inaweza kuwa muhali kutabiri jinsi mlipuko utakavyoendelea. “Siwezi kuzingatia zaidi idadi halisi. Ni vigumu sana kufanya makadirio sahihi ukiwa na data finyu,” alisema.
Kituo Kikuu cha Kudhibiti na Kuzuia Maradhi (CDC) Afrika, Ijumaa kilisema kumekuwa na visa 400 vilivyothibitishwa, ikiwemo vifo 63. Wataalam wanasema huenda kuna visa vingine ambavyo havijagunduliwa wala kuripotiwa.
Ripoti ya CDC inajaribu kukadiria jinsi matukio huenda yakajitokeza, kutegemea masuala mbalimbali – ikiwemo idadi ya maambukizi na vifo ambavyo tayari vimetokea na kasi ya wahusika kugundua na kuwatenga watu walioambukizwa kabla ya kuweza kueneza na kuwaambukiza wengine.
Pillai alisema kiwango halisi cha kutenga hakijulikani lakini kinachukuliwa kuwa “kwenye sehemu chini ya matukio yanayoweza kutokea” yaliyosawiriwa na CDC.
Viwango vya juu vya kuwatenga walioambukizwa, vya asilimia 50 au 70, huenda vikasababisha idadi ya visa kuwa zaidi ya 10,000, walisema maafisa wa CDC.
Lakini ikiwa idadi halisi ya vifo ingekuwa kubwa zaidi mwishoni mwa Mei kuliko inayotambulika sasa, ingesababisha matokeo kuwa mabaya zaidi, walisema. Baadhi ya mifano wakati wa mlipuko mkubwa wa Ebola Afrika Magharibi ilithibitisha mbali sana na uhalisia.
CDC ilitoa takwimu za mifano 2014 wakati mlipuko ulisambaa kupita kiasi na maafisa wa afya kimataifa walichukua hatua upesi kudhibiti. Inakadiriwa katika uwezekano mbaya zaidi ambapo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, watu wasiopungua 1.4 milioni huenda wakaambukizwa. Ilitokea kwamba idadi hiyo ilikuwa mara 50 zaidi ya kilichotokea.
Virusi vinavyosababisha Ebola husambazwa kupitia mtagusano wa majimaji ya mwili kama vile matapishi, damu na shahawa.
Hakuna tiba wala chanjo mahsusi kwa virusi vya Bundibugyo vinavyosababisha mlipuko unaoendelea wa gonjwa sugu la Ebola.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko huu kuwa dharura ya kimataifa Mei.
Baadhi ya wataalam wanaamini maambukizi huenda yalitokea Februari, lakini maafisa wa afya mwanzoni walifanyia vipimo aina tofauti ya virusi vya Ebola.
Mikakati ya kudhibiti mlipuko imekuwa kati ya serikali ya Congo na kundi la waasi linaloungwa mkono na Rwanda, M23, pamoja na kundi linalohusishwa na wanamgambo wa Kiislamu, Allied Democratic Force.
Machafuko yamesababisha maelfu ya watu wanaoishi katika maeneo yanayoathiriwa na ghasia kufurushwa, wanasema maafisa.


from Taifa Leo https://ift.tt/s3RHQMN
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post