Leo ni leo Ol Kalou uchaguzi ukitarajiwa kutambulisha ‘mwenye Mlima’ kati ya Ruto na Rigathi

MATOKEO ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou leo yatatoa mwelekeo wa kisiasa katika eneo lenye idadi kubwa ya wapigakura la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Ni katika eneo hili ambapo chama cha UDA cha Rais William Ruto kilipata ushindi wake wa kwanza wa kisiasa baada ya kushinda uchaguzi mdogo wa wadi ya Rurii dhidi ya Jubilee mnamo 2021. Wakati huo, Dkt Ruto alikuwa na uhasama wa kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya uchaguzi wa 2022. Yamkini historia inajirudia huku uchaguzi wa Ol Kalou ukigeuka pambano la kisiasa kati ya Rais Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Wawili hao wamekuwa na tofauti kali ya kisiasa tangu Bw Gachagua abanduliwe madarakani mnamo Oktoba 2024. Baada ya ushindi wa Rurii, UDA iliendelea kushinda chaguzi ndogo mbalimbali katika Mlima Kenya na pia ikafagia viti vingi 2022 huku Jubilee ikipoteza ushawishi wake eneo hilo. Wandani wa Bw Gachagua wamesema uchaguzi wa Ol Kalou ni nafasi ya kuizika UDA Mlima Kenya na kuizindua rasmi DCP kama chama chenye umaarufu eneo hilo kuelekea 2027. Kwa upande wake, UDA inasema uchaguzi huo ni pambano kati ya siasa za maneno matupu na maendeleo. Chama hicho pia kinasema hata kama DCP itashinda kwa tofauti ndogo ya kura, huo utakuwa ushindi usio na maana kwa kuwa Bw Gachagua amekuwa akidai chama chake kitashinda kwa mwanya mkubwa. Ingawa hivyo, pande zote mbili zimeonyesha imani kuwa zitapata ushindi. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) iliidhinisha wagombea tisa kuwania kiti hicho. Wao ni Sammy Ngotho (DCP), Abdullahi Hussein (Federal Party of Kenya), Kariuki Kamau (People's Renaissance Party), Samuel Muchina (UDA), Edward Mathenge (Kenya Moja Movement) na Rachael Njoroge (People's Democratic Party). Wengine ni Wilson Kigwa (Jubilee), Stephen Wanyoike (National Liberal Party) na Edward Muchiri (Party of National Unity). Mbunge katiika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega, ambaye amekuwa akimpigia debe mgombea wa DCP, alisema ushindi wa chama hicho utathibitisha mwisho wa UDA Mlima Kenya. "Tunasema kifo cha UDA kitathibitishwa Ol Kalou Alhamisi. Hapa ndipo UDA ilizaliwa 2021, na hapa ndipo itazikwa. Siku hiyo hiyo tutakuwa tukisherehekea kuzaliwa kwa DCP Mlima Kenya," akasema. Aliongeza kuwa ushindani ni mkali kwa sababu UDA inataka kuonyesha bado ina ushawishi katika Mlima Kenya. "Ndiyo maana wametumia mamilioni ya fedha na kuzindua miradi ya mabilioni ya shilingi," akaongeza. Matokeo ya uchaguzi huo yanachukuliwa kuwa ya umuhimu mkubwa kwa Rais Ruto na Bw Gachagua kwa kuwa yanatoa taswira jinsi 2027 itakavyokuwa. Iwapo UDA itashinda, Rais ataonekana kama bado ana ushawishi mlimani. Pia utawapa viongozi wa Kenya Kwanza imani kuwa wananchi wanatambua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. Aidha, ushindi huo utapunguza dhana kwamba Mlima Kenya umejitenga na Rais Ruto tangu Bw Gachagua aondolewe madarakani. Isitoshe ushindi unaweza kuvuruga mipango ya upinzani kwa kuonyesha kuwa kutoungana kwao kunarahisishia UDA kazi 2027. Kwa upande mwingine, iwapo UDA itapoteza, matokeo hayo yatafasiriwa kuwa wananchi wa Mlima Kenya wameikataa serikali ya Rais Ruto. Hii ni licha ya kumpa karibu kura milioni tatu katika uchaguzi wa 2022. Kushindwa huko kunaweza pia kuwashawishi viongozi zaidi kuhamia DCP ili kuokoa nafasi wanazoshikilia kisiasa. Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri alisema uchaguzi huo utathibitisha madai ya DCP kuwa imeiteka Mlima Kenya ni uongo. "Matokeo haya yataondoa uongo unaoenezwa kuhusu umaarufu wa DCP. Wamekuwa wakidai UDA imepoteza Mlima Kenya kabisa," akasema. "Hawawezi kudai wanaidhibiti Mlima Kenya hata kiwa watashinda kwa idadi ndogo ya kura. Kwa vyovyote vile sisi tutashinda na mlima si ngome yao," akaongeza. Aliyekuwa Waziri Moses Kuria alisema uchaguzi huo ni mtihani kati ya siasa za matamshi na maendeleo ya kiuchumi. "Nataka kuona kama wananchi wataacha maendeleo na kufuata siasa za maneno. Je, watachagua maendeleo au porojo?" akauliza. UDA iliwatuma wabunge 25 kufanya kampeni huku pia ikipewa usaidizi na sekretarieti ya kampeni iliyoongozwa na Mtaalamu masuala ya kidijitali Dennis Itumbi. Kura ya maoni ya Infotrak iliyotolewa Jumatatu inaonyesha kuwa UDA inaungwa mkono na asilimia tisa pekee katika Mlima Kenya, tofauti kubwa na ilivyokuwa kabla ya uchaguzi wa 2022. Kwa sasa DCP ndiyo chama kinachoongoza kwa asilimia 33 huku asilimia 36 ya wapigakura wakisema bado hawajaamua. Kwa Gachagua, uchaguzi huo ni nafasi ya pili ya kupambana ana kwa ana na UDA baada ya uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr, ambapo UDA ilishinda. UDA pamoja na mshirika wake ODM wamekuwa wakishinda chaguzi ndogo za hivi karibuni katika maeneo ya Mbeere North, Ugunja, Kasipul, Magarini, Malaba na pia kiti cha Seneta wa Baringo. Iwapo Bw Gachagua atashinda Ol Kalou, ushindi huo utathibitisha kuwa bado ana ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya na kuhalalisha madai yake kuwa DCP ndicho chama kikuu katika eneo hilo. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema uchaguzi huo ni suala la "maisha au kifo" kwa DCP. "DCP inataka kuonyesha inaweza kushindana na UDA bila msaada wa chama kingine, " akasema.

from Taifa Leo https://ift.tt/upmx84e
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post