Mshukiwa aliyedaiwa kufa Shakahola ajitokeza kortini

MSHUKIWA anayekabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia pamoja na mhubiri Paul Mackenzie katika kesi ya vifo vya Shakahola, alishangaza Mahakama ya Mombasa baada ya kujitokeza binafsi na kusisitiza kuwa taarifa za kifo chake si za kweli. Moses Karema, anayejulikana pia kama Charif, alisema yuko hai na akapinga ushahidi uliotolewa awali na baba yake mahakamani ukidai alikuwa amefariki akazikwa. "Mimi sijafa. Ilisemekana nimekufa na mwili wangu ukakabidhiwa baba yangu kwa mazishi," Karema aliiambia mahakama. Karema ni mmoja wa washukiwa 95 wanaokabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia kuhusiana na vifo vya wafuasi 238 wa kanisa la Good News International la Mackenzie mwituni Shakahola, Kaunti ya Kilifi. Akiwasilisha utetezi wake, Karema alisema kosa la kutangazwa kuwa amekufa linaonyesha kuwa upande wa mashtaka ulifanya makosa makubwa katika utambuzi wa miili, jambo ambalo, kwa mujibu wake, linadhoofisha ushahidi dhidi yake. Alisema aliitwa kutoka Gereza la Shimo la Tewa kufika Mahakama Kuu baada ya baba yake, Charo Mwathethe Mulewa, kutoa ushahidi katika kesi tofauti ya mauaji ya Shakahola akidai kuwa Karema alifariki, alifanyiwa uchunguzi wa maiti na kuzikwa. Kulingana naye, baba yake alipewa nyaraka zilizoonyesha alikuwa amefariki na akaomboleza na kumzika, kabla ya mahakama kubaini baadaye kuwa alikuwa hai. "Nilitolewa gerezani kwa sababu ilidaiwa nimekufa. Baba yangu alisema alikabidhiwa mwili wangu na hata alikuwa na ripoti ya uchunguzi wa maiti ikionyesha nimekufa na kuzikwa," alisema. Karema alisema ni katika kesi ya sasa ndipo alipoonyeshwa ripoti tofauti ya uchunguzi wa maiti ikionyesha kuwa aliyefariki alikuwa ndugu yake Emmanuel Charo. "Hati niliyoona leo ikionyesha Emmanuel ndiye aliyekufa sikuwahi kuonyeshwa awali. Inanishangaza kuona sasa ni ndugu yangu, si mimi, ndiye anayedaiwa kufa na kuzikwa. Walimfanya baba yangu aniomboleze nikiwa bado hai," alisema. Pia alipinga madai kuwa dada yake Sidi Charo Mwathethe alifariki Shakahola, akisema alikufa miaka mingi kabla hajazaliwa na kuzikwa nyumbani kwao Malindi. Aidha, alikanusha madai kuwa ndugu zake Emmanuel na Winnie walifariki msituni, akisema alipohamia Shakahola mwaka wa 2020 aliwaacha Malindi. Ingawa amekuwa rumande kwa miaka mitatu na hajui walipo sasa, alisisitiza anaamini bado wako Malindi. Karema alikiri kumiliki ekari nne za ardhi Shakahola ambako aliishi na mama yake Ann Kadzo pamoja na dada yake Janet, ambao pia ni washtakiwa wenzake. Alisema hao ndio pekee wa familia yake waliokuwa wakiishi naye na akaomba aachiliwe huru ili arudi nyumbani Shakahola. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulishikilia kuwa, watu watano wa familia ya Karema waliripotiwa kutoweka, huku uchunguzi wa DNA na ushahidi mwingine ukihusisha baadhi yao na miili iliyofukuliwa Shakahola. Ushahidi ulionyesha Karema, mama yake na dada yake Janet walinusurika, huku ndugu zake Sidi, Winnie na Emmanuel wakifariki. Winnie alikuwa akiishi Shakahola na mumewe Alex wa Mashamba. Waendesha mashtaka pia walisema mabaki ya Emmanuel yalitambuliwa na kukabidhiwa familia, lakini baba yake alikataa kumzika kwa vile alitengana na mama yake miaka mingi iliyopita. Hatimaye mabaki yake ambayo yalikuwa mifupa, yalizikwa na mjomba wake. Upande wa mashtaka ulisema, mkanganyiko wa awali ulitokana na baba yake Karema kutambua kimakosa mabaki ya Emmanuel kama ya Karema.

from Taifa Leo https://ift.tt/Z2x6L3c
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post