
NYOTA ya kisiasa ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna inaendelea kung’aa baada ya kumpiku aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i kama mgombea-mwenza anayeshabikiwa zaidi kushirikiana na kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka kama mgombea urais.
Utafiti wa kampuni ya Infotrak jana ulionyesha kuwa kati ya wafuasi wa upinzani, tiketi ya Kalonzo-Sifuna ndiyo inayopigiwa upato zaidi kuliko ya Kalonzo-Matiang’i miongoni mwa wafuasi wa upinzani.
Katika utafiti huo, tiketi ya Kalonzo-Sifuna inashabikiwa kwa asilimia 23 huku ya Kalonzo-Matiang’i ikiwa na asilimia 16.
Asilimia 36 ya wafuasi wa upinzani kutoka Magharibi wanashabikia tiketi ya Kalonzo-Sifuna na kitaifa vijana wa kati ya umri wa miaka 18-26 wanaiunga mkono kwa asilimia 31.
Kwa upande mwingine, ushirika wa Kalonzo-Matiang’i unashabikiwa kwa asilimia 23 eneo la Kaskazini Mashariki na asilimia 22 Mashariki.
Takwimu hizo ndizo za juu zaidi kwa Kalonzo-Sifuna na Kalonzo-Matiang’i kulingana na utafiti huo.
Aidha, utafiti huo unaonyesha tiketi ya Kalonzo-Sifuna ni maarufu katika maeneo yote (mikoa minane ya zamani) isipokuwa Kaskazini Mashariki ambapo Kalonzo-Matiang’i inatamba kwa asilimia 23 dhidi ya 17 ya Kalonzo-Sifuna.
Mbali na mpangilio huo, tiketi ya Matiang’i kama mwaniaji urais na Kalonzo akiwa mgombea-mwenza inashabikiwa na asilimia 15 ya wafuasi wa upinzani huku ya Kalonzo-Rigathi Gachagua ikifuatia kwa umbali kwa asilimia tano pekee.
Tiketi za Gachagua-Kalonzo na Gachagua-Matiang’i zilizoa asilimia nne pekee kila moja.
Kwenye utafiti uliofanywa na kampuni ya TIFA mnamo Mei 14 tiketi ya Kalonzo-Matiang’i ndiyo ilikuwa na umaarufu miongoni mwa wafuasi wa upinzani kwa asilimia 31 huku ile ya Kalonzo-Sifuna ikiwa na asilimia 28.
Kuhusu wawaniaji wa urais, Rais William Ruto anazidi kuwapiku washindani wake kwa asilimia kubwa japo, iwapo uchaguzi ungeandaliwa leo, hakuna yeyote ambaye angeshinda urais katika duru ya kwanza kwa kukosa kufikisha asilimia 50 + kura moja inayohitajika kikatiba.
Katika utafiti huo, Rais alizoa asilimia 32 ya kura ya maoni, akimzidia kwa mbali mshindani wake wa karibu Bw Kalonzo aliyepata asilimia 13. Seneta Sifuna na Matiang’i walifuatia kwa karibu kwa kupata asilimia 12 kila mmoja.
Iwapo Gachagua angewania urais, kulingana na Infotrak, angezoa asilimia nne ya kura, akimzidi Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kwa asilimia moja.
Aliyekuwa Jaji Mkuu, David Maraga angepigiwa kura na asilimia mbili naye Martha Karua wa PLP akapata asilimia moja.
Utafiti huo unaonyesha asilimia 13 ya wapigakura hawajaamua ni mwaniaji yupi wa urais ambaye wangemchagua, hiyo ikiwa na maana kuwa kinyang’anyiro cha urais kingali wazi huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukizidi kukaribia.
Aidha, matokeo hayo yanaashiria kuwa upinzani utalazimika kudumisha umoja hadi debeni ndipo uimarishe nafasi yao ya kumbwaga Rais Ruto.
Kwa jumla, matokeo ya kura ya urais ya utafiti huo yanaonyesha kuwa wawaniaji hao sita wa urais kwa upande wa upinzani wangezoa asilimia 43 dhidi ya asilimia 32 ya Ruto.
Hiyo ni bila kujali mienendo mingine ya wapigakura.
Kimaeneo, Rais Ruto anampiku Bw Sifuna katika umaarufu eneo la Magharibi ambapo ana asilimia 35 huku seneta huyo wa Nairobi akiwa na asilimia 26.
Kung’aa kwa nyota ya Bw Sifuna kunatukia wakati Linda Mwananchi imepanga mikutano miwili mikuwa Trans Nzoia na Bungoma mnamo Julai 25 na 26.
Mikutano hiyo imekuwa ikivumishwa na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya na inatarajiwa kutumiwa na wazee kumtawaza seneta huyo kama msemaji wa jamii ya Waluhya na kumpa baraka ya kusaka urais maeneo mengine.
“Mipango inaendelea na tutatoa maelezo kuhusu mikutano hiyo baadaye,” akasema Bw Natembeya katika mahojiano na Taifa Leo.
Ni katika mikutano hiyo ambapo chama kipya ambacho Bw Sifuna atakitumia huenda kikatangazwa huku nia ikiwa ni kumsawiri kama kiongozi wa kitaifa.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Lumala Masibo, kung’aa kwa nyota ya Bw Sifuna ni hatari kwa Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ambao wametawala siasa za eneo hilo kwa miaka mingi.
“Raila (Odinga) amekuwa akidhibiti siasa za Magharibi na kuwalemea Wetang’ula na Mudavadi lakini sasa Sifuna anaonekana amevalia viatu vya Raila na ushawishi wake unaendelea kupanda. Jinsi ilivyo sasa aidha atawania urais au kuwa mgombeaji mwenza kwa sababu sasa amekuwa mwanasiasa wa kitaifa,” akasema Prof Masibo.
from Taifa Leo https://ift.tt/1rEbqhy
via IFTTT