
WANAWAKE wanazidi kuwa sehemu muhimu lakini isiyoonekana ya mitandao ya wahuni wa kisiasa nchini, huku wakitumika kuhamasisha vijana, kusafirisha silaha kwa siri na kukusanya taarifa za kisiri, utafiti mpya umebaini.
Kwa miaka mingi, macho ya umma yamekuwa yakielekezwa kwa vijana wanaume wanaovamia mikutano ya kisiasa na maandamano wakiwa na rungu na mawe.
Hata hivyo, ripoti mpya inaonyesha kuwa nyuma ya vurugu hizo kuna mtandao uliopangwa vyema unaowahusisha pia wanawake.
Kijana mmoja kutoka Mathare, Nairobi, aliyekubali kuzungumza na Taifa Jumapili kwa masharti ya kutotajwa jina kwa hofu ya usalama wake, alisema wanawake wamekuwa sehemu ya mfumo huo.
“Bila shaka wapo. Huenda wasiwe mstari wa mbele, lakini wanashiriki kikamilifu,” alisema.
Kijana huyo, anayejitambulisha kama mmoja wa "vigogo" wa eneo hilo wanaotafutwa na wanasiasa na wafanyabiashara kuwasaka vijana kwa shughuli za kisiasa, alisema hawabagui wanawake wanapofanya uajiri.
"Sisi ndio viongozi wanaotafutwa na wanasiasa wanapohitaji watu. Hatujali jinsia. Tunawaajiri wanawake, nao pia huleta wengine," alisema.
Kwa mujibu wake, wanawake mara nyingi hawashiriki moja kwa moja katika mashambulizi, bali hujichanganya na umati ili mikutano ionekane kuwa na watu wengi kuliko ilivyo.
Pia hukusanya taarifa, huwatetea wenzao wanapokamatwa na wakati mwingine husafirisha mawe au silaha ndogo wanazofichwa kwenye mikoba yao.
"Kama hujui utakula nini mchana au jioni, huwezi kuanza kuuliza kama mwanamke anafaa kujiunga na kundi au la," alisema.
Hata hivyo, alisema hajawahi kuona mwanamke akifikia kiwango cha kuwa kiongozi mkuu wa mtandao huo, ingawa wengi hutumiwa kuajiri wengine.
Ripoti inayoitwa Goonland: Looking Beyond the Money and Violence in the Political Exploitation of Young Men, iliyoandaliwa na shirika la OdipoDev, inaeleza kuwa magenge ya kisiasa si mkusanyiko wa vijana wasio na ajira pekee, bali ni mtandao wenye viongozi, waajiri, wajumbe na waratibu wanaofanya kazi kwa mpangilio maalumu.
Utafiti huo ulifanywa kupitia mahojiano na wanachama 40 wa magenge ya wahuni, waajiri watano na maafisa watano wa usalama kutoka Nairobi, Mombasa na Kiambu.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mawasiliano hufanywa kupitia makundi ya WhatsApp na vituo vya mitaani, huku fedha na silaha zikisafirishwa kwa siri kupitia watu wanaoaminika.
Wanawake ni miongoni mwa watu hao wanaoaminiwa kusafirisha na kuficha silaha kwa kuwa hawashukiwi kirahisi wakati wa ukaguzi kuhusu usalama.
Mzee wa kijiji cha Mathare, Joseph Ouna, alisema akina mama wachanga wanazidi kuvutwa katika shughuli hizo kutokana na ugumu wa maisha.
"Akina mama hawa wana watoto, na vijana hawa ni marafiki wao. Wanawapa pesa na kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali, hivyo huwa rahisi kuwashawishi wakubali kazi za kisiasa," alisema.
Aidha, alisema baadhi ya wanawake hujitokeza kuwatetea vijana hao wanapokamatwa kwa kuwasawiri kama waathiriwa badala ya wahusika wa vurugu.
Mratibu mmoja wa kisiasa kutoka Kayole ambaye hakutaka kutajwa jina alisema aliwahi kuombwa na mwanamke mwenzake amtafutie vijana kwa shughuli za kisiasa lakini alikataa kwa kuhofia kukamatwa au kushambuliwa.
Alidai pia kuwa rafiki yake mmoja alipelekwa Ol Kalou kuvuruga uchaguzi mdogo uliofanyika eneo hilo.
"Nilimshawishi asiende lakini alikataa. Hadi leo sijui alilipwa kiasi gani," alisema.
Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Nyandarua Central, Kenneth Kiprop, alisema hakuna mwanamke aliyekamatwa kufuatia vurugu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, wala uchunguzi haukubaini wanawake walioshiriki moja kwa moja katika mashambulizi hayo.
Utafiti huo unaonyesha kuwa fedha ndizo kichocheo kikuu cha vijana kujiunga na magenge hayo.
Kuvuruga mikutano ya kisiasa hulipwa kati ya Sh500 na Sh1,500, shughuli za kuvuruga maandamano hulipa Sh500 hadi Sh2,500, huku migogoro ya ardhi ikilipa kati ya Sh500 na Sh2,000.
Hata hivyo, watafiti wanasema si pesa pekee zinazowafanya vijana wabaki kwenye mitandao hiyo. Wengi walieleza kuwa hupata wanatambuliwa, kupata ulinzi, hadhi na hisia ya kuwa sehemu ya kundi.
Ripoti hiyo inaonya kuwa kuanzisha nafasi za ajira pekee hakutamaliza tatizo la magenge ya kisiasa, kwa sababu wanaojiunga nayo hujengewa uhusiano unaotokana na hofu na mshikamano wa kijamii ambao si rahisi kuuvunja.
from Taifa Leo https://ift.tt/8SH94eW
via
IFTTT