Linda Mwananchi yazidi kuvutia wawaniaji mbalimbali uchaguzi ukikaribia

VUGUVUGU la Linda Mwananchi linazidi kubadili sura ya siasa nchini huku likiwavutia wanaowania ugavana kutoka maeneo mbalimbali ya Kenya.
Kilichoanza kama jukwaa la viongozi waliopinga uamuzi wa ODM kuunga mkono azma ya Rais William Ruto kutafuta muhula wa pili, sasa kinaibuka kuwa nguvu mpya ya kisiasa inayojipanga kushindana katika uchaguzi wa 2027.
Chini ya uongozi wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, vuguvugu la Linda Mwananchi limekuwa kivutio kikuu kwa viongozi wanaotafuta ugavana, huku wengi wakisubiri kutangazwa kwa chama ambacho litatumia katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika Kaunti ya Vihiga, Seneta Godfrey Osotsi tayari amejiunga na mkondo huo huku akijiandaa kuwania ugavana baada ya muhula wa Gavana Wilber Ottichilo kumalizika.
Kaunti ya Bungoma nayo imekuwa kitovu cha vuguvugu hilo baada ya Mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi kuhamishia azma yake ya kisiasa huko. Bw Sifuna tayari amemtangaza kuwa mmoja wa viongozi anaoamini na hata kutabiri kuwa gavana ajaye wa Bungoma atatoka Linda Mwananchi.
“Nimekutana na Tim Wanyonyi na viongozi wengine wengi. Ninachoamini ni kwamba gavana wa Bungoma mwaka 2027 atatoka Linda Mwananchi,” alisema Bw Sifuna katika moja ya mikutano yake.
Jijini Nairobi, Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo, ameweka wazi kuwa atamenyana na Gavana Johnson Sakaja katika uchaguzi ujao.
Bw Owino amekuwa akitumia mikutano ya Linda Mwananchi kuimarisha mtandao wake wa kisiasa huku akipata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa vuguvugu hilo.
Seneta wa Kisii, Richard Onyonka pia amejiunga na kundi la wanaotafuta ugavana kupitia Linda Mwananchi. Bw Sifuna tayari amemuidhinisha akisema ana uwezo wa kuongoza Kaunti ya Kisii.
Katika Kaunti ya Kakamega, Seneta Boni Khalwale ameanza kujihusisha zaidi na Linda Mwananchi licha ya hapo awali kuhusishwa na chama chake cha United Patriotic Movement (UPM).
Hatua hiyo imezua hisia kuwa huenda akakitumia chama kitakachozaliwa na vuguguvu hilo kuwania ugavana.
Machakos pia haijaachwa nyuma. Mbunge wa Mavoko, Patrick Makau ameibuka kuwa mmoja wa washirika wakuu wa Linda Mwananchi na tayari ameweka wazi nia yake ya kuwania ugavana wa Machakos mwaka 2027.
Bw Makau ni miongoni mwa viongozi ambao kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka alisema aliwaruhusu kushirikiana na Bw Sifuna katika juhudi za kujenga umoja wa upinzani.
Katika Taita Taveta, Mbunge wa Wundanyi, Danson Mwashako pia ametangaza azma ya kuwania ugavana. Katika mkutano wa hivi majuzi wa Linda Mwananchi, Babu Owino aliwaongoza viongozi wengine kumuidhinisha Bw Mwashako na kuwataka wakazi wa kaunti hiyo kumuunga mkono.
Aliyekuwa Naibu Katibu wa Uratibu wa Jubilee, Pauline Njoroge naye ameweka kando ndoto yake ya kuwania ugavana wa Nairobi na badala yake akaamua kumuunga mkono Babu Owino. Hata amedokeza kuwa yuko tayari kuwa mgombea mwenza wake iwapo mazungumzo ya kisiasa yatazaa makubaliano hayo.
Aliyekuwa Gavana wa Bungoma, Wycliffe Wangamati pia ameanza kujitenga na chama chake cha DAP-K na kutangaza kuwa yuko tayari kutumia chama kitakachozinduliwa na Linda Mwananchi ili kurejea katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Bungoma.
Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, naye amesema atatetea kiti chake kupitia chama kitakachozaliwa na vuguvugu hilo. Bw Sifuna tayari amemtangaza kuwa anayefaa kuendelea kuongoza kaunti hiyo.
Kwa upande mwingine, Gavana wa Siaya, James Orengo, mmoja wa vinara wa vuguvugu hilo ameendelea kutoa ishara zinazochanganya kuhusu mustakabali wake wa kisiasa huku kukiwa na tetesi kuwa huenda akagombea urais au akatetea kiti chake cha ugavana.
Huku viongozi zaidi wakiendelea kuhamia Linda Mwananchi, wachambuzi wanabashiri litakuwa nguvu mpya ya kisiasa itakayoathiri uchaguzi wa ugavana 2027.


from Taifa Leo https://ift.tt/VH6f5Xb
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post