Mawaziri wa Ruto wazozana Wahome akimponda Duale, Kindiki naye akimkemea Ruku

UHASAMA mkali unaendelea kulikumba Baraza la Mawaziri la Rais William Ruto huku mawaziri wake wakijibizana hadharani na kuibua maswali kuhusu uwezekano wa kutekeleza mabadiliko kuelekea kura ya 2027.

Licha ya Rais Ruto kusema akiwa kituo cha kibiashara cha Amagoro, Teso, Busia kuwa hajaanza siasa, mawaziri wake wanaendelea kuzozana huku malumbano yao yakichukua mkondo wa siasa za kikabila.

Uhasama wa ndani kwa ndani umeibua maswali kuhusu uwezo wa baraza hilo la mawaziri kuwajibikia Wakenya ipasavyo, miezi 12 kabla ya kura kuwadia.

Tukio la hivi punde ni majibizano makali kati ya Waziri wa Afya Aden Duale na Waziri wa Ardhi Alice Wahome kuhusu matamshi ambayo Bw Duale anadaiwa kutoa dhidi ya jamii ya Mlima Kenya.

Aidha, Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki ametofautiana vikali na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku kuhusu Mlima Kenya Mashariki kutengana na Magharibi na kujiamulia kivyake mustakabali wake wa kisiasa.

Kwenye video ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii, Bw Duale akiongea kwa lugha ya mama, anadaiwa kulinganisha jamii ya Agikuyu na ya Wasomali kwa kutumia idadi yao nchini huku akidai jamii yake ya Wasomali imekuwa ikibaguliwa na tawala zilizopita za marais Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta wote huku nyingine zikinufaika.

Akiongea katika Kaunti ya Mandera, Bw Duale alilinganisha jamii ya Agikuyu na fisi ambaye hutaka kula kila kitu isitake jamii nyingine zinufaike kwa miradi ya serikali.

Katika video hiyo, Bw Duale alimshukuru Rais Ruto kwa kumaliza kile alichosema ni uongozi ambao umekuwa ukipendelea jamii moja na kubagua jamii nyingine.

Waziri wa Ardhi, Alice Wahome ni kati ya viongozi kutoka Ukanda wa Mlima Kenya ambao sasa wanataka Bw Duale aombe msamaha kwa kauli yake.

Waziri huyo tayari amesema hawezi kuomba msamaha kwa sababu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amewahi kuyatoa matamshi yanayoweza kufasiriwa kama ya kikabila lakini hajawahi kuchukuliwa hatua zozote.

Vilevile Bw Duale amesema kuwa hatafika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) iwapo Bw Gachagua hatafanya hivyo kwanza.

“Makosa mawili hayafanyi jambo liwe sawa na ni mpumbavu tu ndiye asiyebadilisha fikra zake,” akaandika Bi Wahome kwenye mtandao wa X.

Bi Wahome ambaye alihudumu kama mbunge wa Kandara kabla ya kuteuliwa waziri, ni wa kwanza kwenye baraza la mawaziri kumshambulia Bw Duale na kumtaka aombe msamaha.

Mbali na waziri huyo baadhi ya viongozi kutoka Mlima Kenya akiwemo Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba wamemshambulia Bw Duale kutokana na matamshi yake hayo.

Waziri huyo naye amejitetea kuwa matamshi yake, 'Waraabe la-tagis bartay, ka-ridis waa ku dhib', ni methali ya Kisomali wala haikulenga jamii fulani.

“Ujumbe wangu ulilenga kuhakikisha kuna umoja jinsi ambavyo serikali imekuwa ikifanya bila kujali dini au kabila,” akasema Bw Duale.

“Nilenga kuonyesha ugumu wa kumalizwa kwa mtindo ambao upande mmoja umekuwa ukinufaika kwa kipindi kirefu. Sikulenga jamii yoyote au kumdunisha yeyote. Kuna jaribio la kufasiri matamshi yangu visivyo,” akasema.

Uhasama mwingine ulioonekana wazi katika baraza la mawaziri ni ule kati ya Prof Kindiki na Bw Ruku kuhusu Mlima Kenya Mashariki kuwa na mwelekeo wa kisiasa 2027.

Mlima Kenya Mashariki una kaunti za Embu, Tharaka-Nithi, Meru na sehemu ya kaunti za Kirinyaga na inakadiriwa itakuwa na karibu kura milioni mbili mnamo 2027.

Eneo hili limekuwa likipiga kura kwenye kapu moja na wenzao wa Nyandarua, Murangá, Nyeri, Kiambu, Laikipia na Nakuru.

Bw Ruku anasema mtindo huu umefanya wabaguliwe na hata sasa wanaonewa gere kwa kushikilia wadhifa wa Naibu Rais.

“Mimi siwachukii Wakikuyu lakini lazima tufurahie utambulisho wetu. Tulikuwa na majenerali waliopigania uhuru wa nchi kutoka Mlima Kenya Mashariki ndiyo maana tuliwaunga Jomo Kenyatta, Kibaki na Uhuru,” akasema mnamo Juni 30 katika ibada ya Kanisa Kaunti ya Kiambu.

“Haiwezekani kuwa mwana wa kiume kutoka Mlima Kenya Mashariki akifanya kazi na Rais Ruto basi viongozi wa Mlima Kenya Magharibi wanatuambia serikali ni mbaya na tunafaa kutoka. Hatutatoka,” akaongeza Bw Ruku.

Hata hivyo, Naibu wa Rais alionekana kumkemea siku chache baadaye akisema eneo hilo limeungana kwa kipindi kirefu na linastahili kuendelea kufanya hivyo.

“Sitaki watu wazungumze lugha tofauti kwa sababu tumefanya mambo mengi pamoja, tuna historia pevu na hakuna kitu ambacho kitatutenganisha,” akasema Prof Kindiki mnamo Julai 19 wakati wa ibada katika Kaunti ya Embu.

Aidha, Prof Kindiki alikiri kuwa anajikuna kichwa kuhusu unaibu rais ambao unamezewa mate na viongozi wengine kama Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya lakini akasisitiza hawabanduki serikalini.

“Najua tumeongezeka akina Oparanya wamekuja lakini hatuondoki, tutang’ang’ana hapa ndani,” akasema Kindiki.

Wikendi iliyopita, Prof Kindiki aliwachemkia viongozi ambao wanamezea mate wadhifa wake na kumsawiri kama asiyefaa kushikilia wadhifa huo.

“Serikali haiwezi kuwa mzuri wakati naibu rais akitoka upande wao na ni mbaya akitoka hapa. Wakati Uhuru alikuwa rais tulimuunga mkono na hatuwezi kubali jamii ya eneo hilo liongee lugha tofauti,” akasema Profesa Kindiki.

“Ni haki yao kuenda mahali wameenda lakini upande wao wamepangana na namba zote zimeenda na tuko namba 20. Rais Ruto akimaliza muhula wake urais utakuja pande hii,” akasema.

Wikendi viongozi wa ODM kutoka Nyanza na Magharibi walisisitiza kuwa UDA ikiwahi urais naye mgombeaji mwenza anastahili kutoka chama hicho cha chungwa.

“Watu wakuje pole pole na wajue kwamba huwezi kuruka laini. UDA ikipata urais, sisi lazima tupate naibu rais na huyo ni Oparanya,” akasema Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed wikendi akiwa Kakamega.

Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Profesa Lumala Masibo ni wazi kuwa baraza la mawaziri lina vita vya ndani kwa ndani hasa baada ya Profesa Kindiki kuonekana kuanza kuridhiana na Bw Gachagua.

“Baadhi sasa wanamwona kama anayejipanga kivyake na hata alivyoongea wikendi, anaonekana kama mtu ambaye si mtiifu sana kwa Rais tena. Anaweza aje kudai unaibu rais utasalia kwake ilhali si anayeteua mshikilizi wa nafasi hiyo,” akasema Profesa Masibo.

Kauli yake inatokana na hatua ya Bw Gachagua kuwaamrisha viongozi wanaoumuunga mkono wasimshambulie Profesa Kindiki bali wamlenge Rais Ruto moja kwa moja.

“Baada ya Ol Kalou ni dhahiri kuwa Rais amepoteza Mlima Kenya na shida sasa ni kupambania nafasi ya mgombeaji mwenza. Pia baadhi ya mawaziri kutoka Mlima Kenya sasa wanajificha nyuma ya kauli ya Bw Duale kumridhisha Gachagua kwa sababu ya umaarufu wake mlimani,” akaongeza.



from Taifa Leo https://ift.tt/3BdHq0b
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post