
SERIKALI inakaribia kutatua moja ya migogoro ya muda mrefu katika Bonde la Ufa baada ya kuthibitisha kuwa imepata mashamba makubwa katika Kaunti ya Narok ili kuzipa makazi mapya familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau pamoja na watu wengine wasio na ardhi.
Hatua hiyo inalenga kumaliza mateso ya zaidi ya familia 21,000 zilizofurushwa katika oparesheni mbalimbali za serikali ndani ya kipindi cha miaka 21 iliyopita.
Tangazo hilo linajiri huku Rais William Ruto akitarajiwa kuzuru Kusini mwa Bonde la Ufa mwezi ujao.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kuwafidia waathiriwa wa Mau na kuwapa makazi mapya waliokosa ardhi katika Kaunti ya Narok.
Akizungumza Kapkwen, Kaunti ya Bomet, alisema Wizara ya Ardhi inakamilisha taratibu za mwisho na kwamba orodha ya walionufaika itatangazwa hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt Paul Kipronoh Ronoh, pia alisema maagizo ya Rais Ruto ya kuwahamisha waathiriwa hao tayari yanatekelezwa.
“Serikali imefanikiwa kupata ardhi ya kuhamishia familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau katika maeneo ya Narok Kusini na Narok Magharibi pamoja na watu wasio na ardhi Angata Barikoi, eneobunge la Kilgoris,” akasema.
Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, alisema serikali tayari imelipia baadhi ya mashamba hayo na hatimiliki zimekabidhiwa Wizara ya Ardhi.
Pia alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kununua zaidi ya ekari 5,000 zinazomilikiwa na familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, marehemu Isaiah Cheluget, katika eneo la Tendwet, Narok Magharibi.
Kwa mujibu wa Seneta huyo, uhakiki wa majina ya waathiriwa umekamilika na serikali sasa inakamilisha utaratibu wa kugawa fidia na ardhi.
Suala la kufurushwa kwa wakazi wa Mau limekuwa ajenda ya kisiasa kwa zaidi ya miongo miwili.
Tangu 2005, marais na wagombea mbalimbali wameahidi kuwafidia na kuwapa makazi mapya walioathiriwa, lakini ahadi hizo zimekuwa zikicheleweshwa.
Katika muhula wa pili wa Rais Uhuru Kenyatta, maelfu ya familia zilifurushwa tena kutoka maeneo yanayopakana na msitu, huku nyumba, mashamba na mali nyingine zikiharibiwa katika operesheni iliyoongozwa na aliyekuwa Kamishina Ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya.
Rais Ruto amesema serikali yake tayari imelipa familia 2,000 fidia ya Sh300,000 kila moja na imeahidi kuwahamisha jumla ya familia 12,000 ili ziishi maisha ya kibinadamu.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi na wakazi wanasema kiwango hicho cha fedha hakitoshi kununua ardhi wala kujenga nyumba.
“Kiasi cha Sh300,000 hakitoshi hata kununua kiwanja, sembuse kujenga nyumba. Watu walipoteza mashamba, mifugo, mazao na mali nyingine. Wanastahili fidia ya haki,” alisema kiongozi wa eneo hilo Johnstone Kiptanui.
Seneta wa Narok Ledama Ole Kina, ambaye hapo awali aliunga mkono kufurushwa kwa wakazi hao ili kulinda msitu, sasa anasema wakati umefika serikali iwape makazi mapya na fidia kwa kuwa lengo la kuhifadhi Msitu wa Mau.
Hatua ya serikali ya kuharakisha mpango huo inachukuliwa kuwa jaribio la kumaliza mgogoro ambao umeathiri maelfu ya familia na umekuwa ukitumiwa kama ajenda ya kisiasa katika kila uchaguzi mkuu tangu 2007.
from Taifa Leo https://ift.tt/wjBMo9S
via IFTTT