Wakenya kukaza kamba bei za bidhaa zikipanda

Takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha kuwa kiwango hiki cha Julai kinalingana na kile cha Aprili, kikionyesha ongezeko kutoka asilimia 3.8 miezi ya Mei na Juni.

“Ongezeko hilo la bei lilichangiwa zaidi na kupanda kwa bei za bidhaa katika kundi la chakula na vinywaji visivyo na kileo (asilimia 6.8), usafiri (asilimia 4.1), na makazi, maji, umeme, gesi na kawi nyinginezo (asilimia 1.3) kwa kipindi cha mwaka mmoja,” KNBS ilisema.

Aidha, KNBS ilieleza kuwa vinywaji vya pombe, tumbaku na mihadarati vilirekodi mfumuko wa asilimia 5.1 mwezi Julai. Kwa mujibu wa takwimu hizo, mvinyo ndio uliopanda zaidi mwezi huo kwa asilimia 2.1, ukifuatwa na sigara kwa asilimia 0.7 na pombe ya kienyeji kwa asilimia 0.6.

Takwimu za KNBS zinaonyesha kuwa kilo moja ya nyanya iliuzwa kwa wastani wa Sh84.88 kufikia mwisho wa Julai, ikiwa ni ongezeko la asilimia 20.3 ikilinganishwa na Julai mwaka jana.

Kilo ya mahindi bichi pia ilipanda bei kwa asilimia 18.4 hadi Sh71.24.Bei ya mahindi kwa jumla imepanda kwa asilimia 17.5 hadi Sh75.88 katika kipindi hicho cha miezi 12.

Bidhaa nyingine zilizoshuhudia ongezeko la bei kwa zaidi ya asilimia 10 na kilo ya machungwa (asilimia 16.1), karoti (asilimia 17.7) na sukari (asilimia 13.6).

Kati ya Juni na Julai, mafuta ya taa ndiyo yaliyoongoza kwa ongezeko la bei, ikipanda kutoka Sh147.92 hadi Sh157.76 kwa lita moja. Bei ya petroli pia ilipanda kutoka Sh178.19 hadi Sh187.37 kwa lita, ikiwa ongezeko kubwa la gharama ya mafuta.

Ingawa mfumuko wa bei wa asilimia 4.1 bado uko ndani ya lengo la serikali la kati ya asilimia 2.5 na 7.5, wachambuzi wameonya kuwa endapo ongezeko la bei ya mafuta litaendelea, huenda mfumuko wa bei ukaongezeka zaidi.

Mwezi uliopita serikali ilifichua kuwa hazina ya ruzuku ya kupunguza bei ya mafuta ilikuwa imeisha, hali iliyowaacha watumiaji katika hatari ya mabadiliko ya bei duniani ambayo yamesababisha gharama ya dizeli na petroli kupanda kwa angalau Sh8.67 kwa lita.

Kwa miezi miwili mfululizo tangu Mei, serikali haijaweza kutumia ruzuku hiyo, hali ambayo imesababisha kupanda kwa gharama ya bidhaa nyingi kama vile usafiri, chakula na kawi.

TAFSIRI: BENSON MATHEKA

from Taifa Leo https://ift.tt/H5ByOaA
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post